Monday, August 18, 2014

"UKAWA ni kikundi kidogo cha watu waliojipanga kuvuruga AMANI ya nchi"

Demokrasia bila mipaka ni ukichaa na demokrasia bila nidhamu ni uwendawazimu" Mwl Jk Nyerere
Ndugu zangu Watanzania, naomba mfahamu kuwa miongoni mwa wajumbe wote wa bunge la katiba takriban 600, wajumbe waliofanya maamuzi haramu ya kugomea ni 79 ambao ni pungufu ya asilimia 15% ya wajumbe wote, na sio kweli kuwa wao pekee ndio wenye tafsir sahihi ya rasimu.(Martha Magessa)

Wajumbe wa makundi mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa vyama vyote vya siasa takriban 18 kati ya 22 bado wamo kwenye bunge, kati ya wajumbe wa kundi la 201 walioasi ni 15 ambapo bara ni 9 na zanzibar 6 lakini pia katika wanaojiita UKAWA wapo wabunge ambao wameendelea kurudi bungeni kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.
Takwimu hizi zinatuthibitishia kuwa UKAWA ni kikundi kidogo cha watu waliojipanga kuvuruga AMANI ya nchi, watu ambao hawataki KATIBA wala hawataki MUUNGANO.
Ndugu zangu watanzania, naomba leo niwape picha na kilichopo nyuma ya pazia ya kikundi hiki kiitwacho ukawa ambacho kinaratibiwa na viongozi wachache na maslahi yake kujulikana kwa wachache zaidi tena yaliyojikita katika misingi ya kibinafsi.
Mfano, ndoa ya CUF na CHADEMA inayopelekea NCCR mageuzi kuwa bendera fuata upepo imejengwa katika misingi ya kuvunja muungano, kwa makubaliano kuwa CUF kubaki na Zanzibar na CHADEMA kubaki na Tanganyika. CUF inataka inufaike na mkakati dhalimu wa kunyonya rasilimali za wazanzibar yakiwemo mafuta bila kushurutishwa na sheria za muungano kwani wakiamini kubaki na muungano imara CUF na viongozi hao wachache katika chama hicho wanakosa fursa za kupora rasilimali za wazanzibar.
Ikubumbukwe Muungano ndio unalinda mipaka na usalama wa raia katika kujiendeleza na kujinufaisha bila ubaguzi wa kikundi cha watu wachache ambacho kinaenda kinyume na utawala wa sheria.
Ikumbukwe kuwa rasimu ya CUF walioipeleka kwa Mhe. Raisi mwaka 2011, mapendekezo yao ni tofauti na madai yao sasa ya serikali 3, hapa inatosha kutupa picha kuwa nia yao ni kuvunja muungano ili watuache katika mfarakano kama nchi nyingine zinazoteseka kwa sababu ya wanasiasa uchwara.
Ifahamike ajenda ya CHADEMA ni kuvunja muungano ndio maana CHADEMA hawahangaiki kuimarisha chama Zanzibar, nia yao ni kubaki na Tanganyika ili waigawe Tanganyika katika vipande vipande kwa lugha ya majimbo ili adhima yao ya ukanda na ukabila itimie. Moja ya kanda yao ambayo wametangaza katika kanda 8 walizo nazo ni Kilimanjaro, tanga, arusha na manyara.
CHADEMA ina amini kanda hii inajitosheleza kwani ina bandari,bunga za wanyama,madini, milima . Na hii imepelekea mbunge mmoja wapo wa CHADEMA kulazimika kusema kaskazini ni nchi huru huku mwenyekiti wao Mbowe akiendelea kudai mapato ya mlima Kilimanjaro yabaki Kilimanjaro.
Katika kipindi hiki ambacho wenzetu wamegomea bunge la katiba ambalo lipo kisheria na madai yao yakibadilika kila kunapokucha tena yakiwa na upotoshaji mkubwa kwa kufanya siasa chafu ili mradi watimize azma ya kuisambaratisha Tanzania wakiwa makuwadi wazuri wa soko huria. Ukihoji leo sababu iliyowafanya watoke bungeni ni tofauti kabisa na sababu waliyoitoa siku wanatoka bungeni, eti msingi wao mkuu wao ni watetezi wa wananchi.
Lakini tumesikia katika vyombo mbalimbali wananchi hao wakiwaasa na wakiwataka warejee bungeni ili kukamilisha kazi ya kisheria na tumaini la watanzania la kuwapatia katiba mpya.
UKAWA hawa bila haya wamekataa. Swali..? wanamtumikia nani. Mpaka sasa imepelekea wananchi hao wanaosema wanawawakilisha wameamua wenyewe kuja Dodoma kuendelea kusema kero zao na shida zao ili katiba hii iweze kutoa majawabu, mfano tumeshuhudia makundi ya wakulima, jukwaa la wahariri wa vyombo vya habari, wafugaji na makundi kadha wa kadha yameendelea kutiririka Dodoma.
Hii ni picha tosha kuwa UKAWA hawawatumikii watanzania na wameamua kuwahadaa watanzania kwa mgongo wa kuwatetea huku ajenda yao ikiwa maslahi binafsi.
Ndugu zangu watanzania tunapowaunga mkono watu wanaoendelea kuligomea bunge la katiba wakati tunajua nchi inaongozwa kwa utawala wa sheria, na wao ndio wamevunja sheria, tujue kabisa kuwa tunaenda kinyume na utawala bora, ambao umejengwa kwenye msingi wa sheria na demokrasia. Msingi wa demokrasia sio kususa baada ya kushindwa hoja, UKAWA hawataki hoja za wengine na wanalazimisha hoja zao pekee ndizo zikubalike kinyume na msingi wa demokrasia. Na bila haya watu hao wasiojua demokrasia wameendelea kuwashawishi watanzania waingie barabarani huku wakijua kuwa Katiba haipatikani barabarani kama wanahoja kwanini wanaikimbia Dodoma..? Mchakato huu ulianza kisheria na utahitimishwa kisheria, sio matamko ya makuwadi wa soko huria.
Miongoni mwa madai yao matatu, (i) Rais avunje bunge (2) kinachojadiliwa Dodoma sio rasimu ya warioba (3) Serikali tatu ndio maendeleo
Kwa ujumla wake, UKAWA wanajua mamlaka ya Rais kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011, sura namba 83 imempa Rais mamlaka ya kuunda tume, kuchagua wajumbe 201, kutangaza na kuitisha bunge na kuzindua bunge la katiba, kupokea katiba inayopendekezwa na kuitangaza kwenye gazeti la serikali.,kwanini wanataka kumlazimisha Rais kuvunja Sheria kwani hayo niliyoyataja ndio ambayo Rais anayo mamlaka ya kisheria kuyafanya katika mchakato huu wa Bunge la Katiba, na ndio maana hata wale wajumbe aliowateua ambao wamegomea Rais hajawatengua.
,kinachojadiliwa bungeni ni Rasimu ya jaji warioba na kiko wazi, kwa sababu msingi mkuu wa majadiliano ni Rasimu inayotokana na tume tena kwa mujibu wa Sura namba 83 kifungu cha sheria namba 25/26 na kwa mujibu wa kanuni za bunge kifungu namba 33 (8). Wanajua mamlaka ya bunge na waliohusika kutengeneza sheria hizi pamoja na kanuni waache kuwahadaa watanzania.
Jambo la mwisho lenye kusikitisha zaidi ni kung'ang'ania Serikali tatu kana kwamba ndio kilio kikubwa cha watanzania, naomba niulize swali kati ya Muungano na migogoro ya ardhi ni jambo lipi limepoteza maisha ya watanzania wengi na ambalo tunatakiwa kulifanyia kazi ili watanzania wasiendelee kumwaga damu. Kati ya tatizo la ajira na muungano, kati ya afya na muungano, kati ya maji salama na safi na muungano, kati ya elimu bora na muungano, kati ya haki za binadamu na muungano eti watu hawa wanaojiita ukawa kwao muhimu muungano kuliko chochote kile.Watanzania naomba tupime kama ni kweli kuwa hawa ni watetezi wetu au ni makuwadi wa soko huria.
Kwa niaba ya watanzania wazalendo, napenda kuiomba serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama kuwatupia UKAWA jicho la pekee katika kuangalia na kufuatilia kwa ukaribu zaidi nyendo za UKAWA na hata kutuambia ni nani wako nyuma yao kiasi cha kuwa na kiburi cha kupindukia. Wito wa watanzania kwa vyombo vya ulinzi na usalama ni kuwa amani, umoja na uhai wa nchi hii uko mikononi mwao, kwani nia ya UKAWA sio nzuri kwa mustakabali wa taifa hili na lazima wakumbuke USIPOZIBA UFA UTAJENGA UKUTA na pia MAJUTO NI MJUKUU NA HUJA BAADAE. UKAWA wanataka kutengeneza Misri, Afrika ya Kati, Libya, Syria, Sudani Kusini nyingine hapa Tanzania.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika
PAUL MAKONDA
Katibu , idara ya Hamasa na chipukizi
Jumuia ya vijana chama cha mapinduzi (UVCCM)

No comments: