TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Siku ya Vijana Duniani itafanyika
tarehe 12 Agosti, 2014 ikiwa na lengo la kuyafanya masuala mbalimbali ya
vijana kutambulika katika jamii ya Kimataifa. Mwaka huu, ujumbe ni “Vijana na Afya Kiakili”.
Tarehe hii iliamuliwa kuwa Siku ya
Vijana Duniani na Umoja wa Mataifa mwaka 1999. Hii ni Siku maalum
inayodhihirisha kutambua kazi muhimu zinazofanywa na vijana na umuhimu
wake katika jamii pamoja na kuwapa fursa kwa ajili ya kuongeza ufahamu
juu ya changamoto na matatizo yanayoukabili ulimwengu wa vijana.
Mijadala katika maeneo maalum
pamoja na taarifa juu ya kampeni mbalimbali zitafanyika katika maeneo na
nchi mbalimbali ulimwenguni kwa ajili ya kutoa hamasa kwa nchi
wanachama pamoja na jamii ili kuelewa mahitaji ya vijana, utekelzaji wa
sera mbalimbali katika kusaidia kupambana na changamoto zilizopo, pamoja
na kuwasaidia vijana kushiriki katika michakato ya utoaji wa maamuzi.
Siku ya Vijana Duniani ni kutambua
na kuthamini kuwa kipindi cha ujana kinaambatana na mabadiliko makubwa
na ya haraka na safari ya kutoka utotoni kufikia utu uzima inaweza kuwa
ngumu na yenye changamoto nyingi na hivyo kuhitaji utulivu na ukomavu wa
akili. Kwa Tanzania kijana ni mtu yeyote mwenye umri kati ya miaka 15
hadi 35.
Katika Siku hii na siku za mbeleni
itakuwa fursa ya kuweza kutoa ufahamu juu vikwazo mbalimbali
vinavyowakabili vijana ikiwemo kunyanyapaliwa na kubaguliwa, lakini pia
kuwapa vijana nguvu ili waweze kutimiza malengo yao.
Tanzania kama sehemu ya duania
inatambua na kuthamini changamoto maalum zinazowakabili vijana walioko
katika mazingira hatarishi pamoja na umuhimu wa kuhakikisha kuwa
wanahusishwa kikamilifu katika malengo ya maendeleo katika ngazi ya
kitaifa na kimataifa.
Tanzania itaendelea kufanya kazi
kwa karibu na vijana pamoja na wadau wa maendeleo ili kuunga mkono
programu za elimu ya afya kwa vijana walioko ndani na nje ya shule,
walioko katika taasisi za mafunzo rasmi na zisizo rasmi ili kukuza uwezo
wa taarifa na mawasiliano ya kisasa.
Katika ngazi ya kitaifa Tanzania
imedhamiria kukuza na kuboresha misingi ya kuwashirikisha vijana katika
maeneo ya sera mbalimbali, programu ya mikakati ya maendeleo ya vijana
ambapo lengo ni kuhakikisha kuwa sauti zao zinasikika na kufanyiwa kazi.
Katika kutekeleza eneo hili
Tanzania inalenga kuweka fursa zitakazowawezesha vijana kukuza utaalamu
na ujuzi utakaowawezesha kufanikiwa katika kipindi cha mpito kutoka
ujana kwenda katika utu uzima kwa kuzingatia hali halisi ya mabadiliko
makubwa yanayoendelea kutokea duniani.
Kwa kutambua umuhimu huu, Wizara
ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inatumia fursa hii kuwakaribisha
vjana pamoja na wadau mbalimbali katika Maonyesho ya Wiki ya Vijana
Kitaifa ya mwaka huu ambayo yatafanyika Mkoani Tabora kuanzia tarehe 08 –
14 Oktoba ikiwa ni mwedelezo wa kuwapa vijana na wadau taarifa
mbalimbali kuhusiana na maendeleo kwa ujumla wake.
Tukiwa tunasherehekea Siku ya
Vijana Duniani Wajibu wetu mkubwa ni kuona kuwa vijana wanashiriki
kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika jamii
wanazoishi.
Katika Siku hii Vijana wote
wanakaribishwa kuandaa hadithi mbalimbali fupi zenye mafunzo, mashairi,
picha mbalimbali, video na kazi za sanaa ili kazi itakayoonekana inafaa
iweze kuwa miongoni mwa kazi zitakazojumuishwa katika Chapisho la Umoja
wa Mataifa ‘Kuwajumuisha Vijana Kijamii kwa kuzingatia Afya Kiakili’.
No comments:
Post a Comment