Tuesday, October 7, 2014

KURA YA MAONI, NI TURUFU YETU WANANCHI, TUSIICHEZEE

Mwandishi Eric Shigongo

NIWASALIMU wote kwa jina la Mwenyezi Mungu, kwani bila yeye hakuna lisilowezekana. Nimekuwa nikiwahimiza siku zote ndugu zangu, bila kujali imani mbalimbali za dini tunazoziabudu, tutenge muda kwa ajili ya kumshukuru Mungu, kwa sababu yeye ndiye kila kitu.

Sisiti kurudia, tena na tena kusisitiza kuwa tuko hivi tulivyo leo kwa sababu ya mapenzi yake, kwa sababu kama angetaka, wewe usingepata muda wa kusoma maandishi haya, ama ungekuwa umeshakufa, au uko katika hali mbaya ukiteseka. Lakini yeye kwa mapenzi yake, amekufanya uwe na amani na mzima wa afya.
Lakini siyo kwetu tu tuliopewa afya leo, hata wale walio katika mateso, mitikisiko na manyanyaso, bado wanapaswa kumuomba Mwenyezi Mungu kwa sababu anao uwezo wa kuondoa maumivu waliyonayo, kama tu wataamini katika yeye.
Baada ya kusema hayo, naomba sasa nije kwenye mada yangu ya leo. Wiki iliyopita niliandika kuhusu umuhimu wa busara kutumika wakati wa kumalizia mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya, uliokuwa ukiendelea mjini Dodoma ambao ulikuwa katika hatua zake za mwisho.
Ninashukuru Mungu kwamba kazi ile kubwa na muhimu kwa taifa letu ilifanyika na kukamilika, licha ya changamoto za hapa na pale maana kesho, Rais Jakaya Mrisho Kikwete atakabidhiwa rasmi rasimu ya katiba hiyo kwa hatua zaidi zinazopaswa kuendelea.

Kwa kuwa jambo hili limekuwa ni muhimu sana kwa taifa letu, sina budi kuendelea tena kulizungumzia, kwa sababu kitu hiki kama hatutakwenda nacho sawa, ipo hatari ya kuigawa au hata kuisambaratisha nchi yetu ambayo kwa kipindi chote tokea uhuru tumekuwa na amani, upendo na mshikamano unaowanyima raha maadui zetu.

Hatua itakayofuata baada ya Rais Kikwete kukabidhiwa katiba hiyo ni kwa wananchi kupiga kura ya maoni ya kuikubali au kuikataa. Ingawa kwa macho ya kawaida inaonekana kama ni kitu chepesi na kitakachokwenda vizuri, ni vyema tukakumbushana kwamba kama hatutakuwa makini, tunaweza kujikuta tukianza utengano wakati au baada ya zoezi hilo.

Kura ya maoni ni kura kama zilivyo kura zingine na hatimaye mshindi anapatikana. Tofauti ya ushindi wa kura ya maoni na chaguzi zingine ni kwamba mshindi wa kura ya maoni siyo chama cha siasa, bali ni Watanzania wa makundi yote, wenye vyama na wasio na vyama.
Tusikae tukafikiri kwamba wanaopaswa kupiga kura hii ni wana CCM, Chadema, CUF au NCCR-Mageuzi. Hapana, Mtanzania yeyote aliyefikisha umri wa kuanzia miaka 18 ana haki na kimsingi anatakiwa kuipigia kura katiba hii.

Lakini wakati tukijiandaa kupiga kura ya kuikubali au kuikataa, ni vizuri pia tukajipa muda wa kujua kitu tunachokwenda kukichagua. Pamoja na kwamba kila makundi, yawe ya kidini, kiharakati, wanasiasa, kijamii na kadhalika yana viongozi wao, lakini ni jambo jema sana kwa kila mtu mmoja mmoja kujiridhisha na anachokiamini badala ya kufuata mkumbo.

Katiba hii inashikilia uhai wako, iangalie kama itakutendea haki au la. Ukiona haki zako nyingi za msingi zimewekwa pembeni, ikatae hata kama kiongozi wako atasisitiza kuwa ni nzuri na inakufaa. Ukiona mambo mengi unayoyaamini yapo, huna sababu ya kuikataa.

Binafsi ninawaheshimu viongozi wa makundi yote, kuanzia ya kidini, wanaharakati wa haki za binadamu, wanasiasa na kijamii, lakini ni lazima niwe mkweli kuwa mwisho wa siku, ningependa kila Mtanzania apige kura ya maoni kwa kuzingatia utashi wake binafsi yeye kama mwananchi na siyo kwa utashi wa viongozi wa makundi tajwa.

Viongozi wamefanya kazi kubwa sana wakati wa mchakato na hata sasa tunapoelekea kwenye kura ya maoni. Hapa tulipofikia ni wakati muafaka sasa wa wananchi kuachiwa wafanye uamuzi wa mwisho.
Ninafahamu wapo baadhi ya viongozi wetu, pengine kwa nia njema au hila, wamekuwa wakitaka wananchi wawasikilize na kuwafuata kwa kila wanachokisema kuhusu katiba.
Ni kweli kwamba wao wana ufahamu mpana kidogo kuhusu katiba pengine kuliko wananchi, lakini siyo jambo zuri kuwalazimisha kufuata matakwa yao, wakati kilichomo ndani ya katiba hiyo ni vitu vyao wanavyopaswa kuvijua na kuvielewa vizuri kabla ya kukubali au kukataa.

Lengo langu hapa ni kutaka wananchi wajue kuwa kukubali au kukataa kupitisha katiba inayopendekezwa maana yake ni kuwa kama itakuwa ni mbaya halafu wao wakaikubali, watateseka nayo kwa miaka mingi ijayo na hawatakuwa na jinsi tena ya kubadili kwa sababu wakati huo hautakuwepo.
Lakini bahati mbaya zaidi ni kuwa wanaweza kuikataa katiba ambayo ina mambo mazuri sana kwa ajili ya ustawi wetu kama taifa na hata kwa mtu mmoja mmoja, kwa sababu tu tutakubali kuwasikiliza viongozi wetu wa dini, siasa au makundi mengine ya kijamii.
Nimalizie kwa kuwasisitizia tena wananchi wenzangu, kabla ya kwenda katika sanduku la kura, tuwe tumejua nini tunataka, tujiondoe kuwa katika kundi la wafuata mkumbo. Msikilize kiongozi wako lakini uamuzi wa mwisho uwe wako!

No comments: