Tuesday, December 30, 2014

HABARI KUTOKA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

tff_LOGO1
AZAM, MTIBWA, SIMBA, YANGA KUCHEZA MAPINDUZI

Timu za Azam, Mtibwa Sugar, Simba na Yanga zitashiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi inayofanyika kisiwani Zanzibar kuanzia Januari 1 hadi 13 mwakani.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa ruhusa kwa timu hizo kucheza mashindano hayo baada ya kuhakikishiwa na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) kuwa kesi iliyofunguliwa dhidi ya viongozi wake imeondolewa mahakamani.

Kutokana na timu hizo kushiriki Kombe la Mapinduzi, mechi zao za raundi ya tisa na kumi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zitachezwa katikati ya wiki baada ya kumaliza mechi zao za michuano hiyo.
Hivyo mechi za VPL ambazo hazitachezwa wikiendi hii ni kati ya Azam na Mtibwa Sugar, Mbeya City na Yanga, na ile kati ya Mgambo Shooting na Simba. Mechi za wikiendi ijayo zinazopisha michuano hiyo ni kati ya Kagera Sugar na Azam, Coastal Union na Yanga, Mbeya City na Simba, na Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons.
18 WAPATA BEJI ZA UAMUZI FIFA
Waamuzi 18 wa Tanzania wamepata beji za uamuzi za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwa mwaka 2015.
Idadi hiyo ambayo ni rekodi kwa Tanzania inahusisha waamuzi saba wa kike. Waamuzi wa kati wa kike waliopata beji hizo ni pamoja na Jonesia Rukyaa Kabakama aliyechezesha mechi ya Nani Mtani Jembe kati ya Simba na Yanga. Wengine ni Florentina Zablon Chief na Sophia Ismail Mtongori.
Waamuzi wasaidizi wa kike waliopata beji hizo ni Dalila Jafari Mtwana, Grace Wamala, Hellen Joseph Mduma na Kudura Omary Maurice.
Kwa waamuzi wa kati wa kiume ni Israel Mujuni Nkongo, Martin Eliphas Sanya, Mfaume Ali Nassoro na Waziri Sheha Waziri. Waamuzi wasaidizi ni Alli Kinduli, Ferdinand Chacha, Frank John Komba, John Longino Kanyenye, Josephat Deu Bulali, Samuel Hudsin Mpenzu na Soud Iddi Lila.

No comments: