WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka
akizungumza na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Hyyat Kilimanjaro
jijini Dar es salaam leo kuelezea mambo mbalimbali kuhusu Akaunti ya
Escrow.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa wamefurika katika mkutano huo.
Baadhi ya wapiga picha wa vyombo mbalimbali vya habari wakiwajibika kupata picha katika mkutano huo.
…………………………………………………………………………………………………………
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka amesema kamwe awezi
kujiuzulu wadhifa wake kwa kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow
iliyomkumba kwani tukio alilolifanya ni la mafanikio makubwa kwa upande
wa shule zake.Alisema kitendo cha yeye kufanikiwa kuomba na kupokea
shilingi zaidi ya bilioni 1.6 kama mchango kwake ni mafanikio makubwa
kwa kufanikisha kupata mchango wa kuendesha shule za Sekondari ya
Wasichana ya Barbro ya Jijini Dar es Salaam pamoja na Shule ya Wasichana
ya Kajumulo ya Mjini Bukoba, hivyo haoni sababu ya kuachia nyadhifa
zake.
Profesa Anna Tibaijuka ametoa
kauli hiyo mapema leo jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya
mazungumzo na waandishi wa habari kuendelea kutolea ufafanuzi juu ya
sakata hilo lililoitingisha Serikali. Hata hivyo bado anaamini fedha
alizopokea ni fedha safi kwani zimetolewa wazi na kwa nia njema na
mchangaji wa fedha hizo.
“…Kama Serikali itabainisha kuwa
fedha hizo ni haramu basi nitazirejesha Serikalini. Nafanya vitu vingi
lakini havionekani na kusisika…naomba tusiwe watu wa kuhukumu bila
kumsikiliza anayetuhumiwa
ni dhambi tena dhambi ya mauti.
Binafsi bado nashangaa kwanini Kamati ya Zitto (Mwentekiti wa Kamati ya
Hesabu za Serikali) haikuniita kunisikiliza, Kamati ya Zitto kwanini
haikuniita kujitetea,” alisema Prof. Tibaijuka.
Alipoulizwa haoni fedheha
kuandamwa na kashfa hiyo na kwanini asijiuzulu kulinda heshima yake na
wapigakura wake, alisema haoni fedheha yoyote kwake wala kwa wapiga kura
wake. “…Mimi naona ufahari wewe unasema fedheha wewe vipi…labda fedheha
itakuja baada ya kubainika aliyetuchangia fedha hizo kaziiba.
Akizungumzia mchango huo wa
zaidi ya bilioni 1.6 aliopokea kutoka kwa Mfanyabiashara James
Rugemalira wa Kampuni ya Mabibo Beer Wines and Spirits ambao ni fedha
zinazodaiwa kuchotwa kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow, anasema ni mchango
mkubwa ambao hata yeye baada ya kuuona alishtuka na kushukuru sana kwa
mtoaji.
“…Kwa kweli ulikuwa mchango
mkubwa hata mimi nilishtuka pia na kushukuru sana, baada ya kuuona
tulianza kupeana taarifa kuwa kuna neema imetokea. Hata hivyo si sawa
kitendo cha baadhi ya watu na vyombo vya habari kuwaaminisha wananchi na
taifa kuwa tumeiba fedha hizo, ukiangalia utabaini kuwa hata mimi
nimejikuta kwenye mgogoro wa Escrow bila kujua kutokana na kuhangaika
kutafuta fedha za wafadhili kwenye shule yetu.
“…Mimi ni mbunge lakini sikupewa
nafasi ya kujitetea kwenye sakata hili, sasa tuache kuwaaminisha
wananchi propaganda mbaya tena ya uhaini. Uandishi huu wa kiupotoshaji
sio mzuri ni kupotosha jamii. Kimsingi wananchi wanaitaji taarifa za
ukweli na si habari za udaku.” alisema Profesa Tibaijuka ambaye amegoma
kabisa kujiuzulu.
Anasema kitendo cha wanahabari
kuandika kwamba amechota fedha za Escrow ni upotoshaji kwani yeye
hakufanya hivyo. Sasa mi nasema wananchi wangu ambao wanateseka kule na
kilimo alafu wanasikia nimechota fedha za Escrow wanajisikiaje kwa hili.
Kwa hiyo nimekuja hapa kufafanua ili jambo ili lieleweke kwa kweli mimi
kama waziri sihusiki katika miamala iliyofanyika. “Wanasema ukweli
ukidhihiri uongo utajitenga nimeona kwamba nitoe ufafanuzi.
No comments:
Post a Comment