CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetaka
watendaji wote waliosababisha kuharibika kwa uchaguzi wa Serikali za
Mitaa katika baadhi ya maeneo nchini wachukuliwe hatua kali.
Kimesema, watendaji hao
wanastahili kuchukuliwa hatua kali kwa sababu kilichotokea ni uzembe wa
hali ya juu uliofanyika huku ikifahamika wazi kwamba tukio la uchaguzi
huo ni kubwa na muhimu sana kwa taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es
Salaam, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye (pichani) amesema,
kulingana na kosa lililojitokeza kuwa la wazi hakuna haja ya kupoteza
fedha na muda kufanya uchunguzi kabla ya kuwachukulia hatua waliohusika.
“Kwa mfano, Mkurugenzi wa
Halmashauri ana kila kitu na alijua mapema kuwa uchaguzi utafanyika lini
kwa kuwa halikuwa jambo la dharura, inakuwaje anaruhusu karatasi ziende
kwenye vituo zikiwa zimechapishwa hovyo au mahali pengine vifaa viwe
vicheche?” alihoji Nape na kuongeza “Sasa hapa unahitajika uchunguzi
gani tena kubaini aliyevurunda?”.
“Mahali pengine zimefika karatasi
za kupigia kura jina la mgombea wa CCM nembo ya CUF, au mgombea wa CUF
nembo ya CCM! huu ni uzembe wa hali ya juu sana na adhabu yake
haistahili kusubiri uchunguzi”, alisema Nape.
Akizungumzia matokeo ya awali ya
Uchaguzi huo, Nape alisema licha ya vyama vya upinzani kuwa na umri wa
miaka 22 sasa, huku vikifanya harakati za kujaribu kuungana katika umoja
wanaouita Ukawa, bado CCM imewagaragaraza vibaya.
Nape amesema, katika uchaguzi huo,
CCM imepata zaidi ya asilimia 80 ya ushindi kwa nchi nzima, huku Dar es
Salaam, ikiwa na asilimia zaidi ya 70 licha ya kwamba Chadema wanao
wabunge wawili katika mkoa huo.
“Katika mazingira ya sasa ambayo
vyama vya upinzani vina miaka 22, na vinafanya hata harakati za kujaribu
kuungana, asilimia 80 si ndogo kwa CCM, na tunaamini huu ni mwanzo
mzuri, na hatuoni namna ambavyo asilimia hii itabadilika katika uchaguzi
mkuu mwakani, maana uchaguzi huu ni kama kura za maoni”, alisema Nape.
“Wanaosema, asilimia ya CCM
imeshuka, wajue kwamba tuliposema tunataka mfumo wa vyama vingi maana
yake tulitaka ushindani katika demokrasia, katika demokrasia ya
ushindani ni vema kuruhusu vyama vya upinzani vikakua ili ushindani huo
uonekane”, alisema Nape nakuongeza.
“Hata hivyo inasikitisha kwamba
licha ya vyama vya upinzani kuwa na umri wa miakaa 22 sasa, bado
havijaweza kujenga imani ya kutosha kwa Watanzania kuwa vinaweza
kuongoza, lazima wapinzania wazidi kujijenga ili Watanzania wawaamini,
asilimia hii 14 waliyopata karika uchaguzi huu wa serikali za mitaa bado
ni ndogo sana kwa uhai wa miaka hiyo”.
Amesema, asilimia iliyopata CCM
wakati matokeo mengine yakisubiriwa ambako uchaguzi uliahirishwa, ni
dalili za wazi kwamba, Ukawa bado ni muungano wa mashaka kwa sababu kama
wangeungana na kuachiana maeneo ni kweli wangeweza kufika mbali.
“Hebu jiulizeni na ninyi, kama
kweli UKawa ulitumika vema, ni kwa nini kwenye karatasi za matokeo ya
uchaguzi huu, kila chama kina mtu wake na idadi ya kura alizopata? Kwa
nini zisiwe za mgombea mmoja wapo wa Ukawa?… Hii inamaanisha ndoa hii ya
ukawa bado sana”, alisema Nape.
Nape aliwashukuru wananchi nchini
kote kwa kuendelea kuiamini CCM, na kuchagua wagombea wake, huku
akivipongeza vyama vya upinzani kwa maeneo waliyochaguliwa, akiwataka
kuchapa kazi vinginevyo siku za baadaye wananchi watawahukumu kwa
kuwatosa.
Katibu wa NEC, Itikadi na
Uenezi, Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari, leo katika Ofisi
Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, kutoa
tathmini ya matokeo ya awali uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika
juzi nchini kote.
Katibu wa NEC, Itikadi na
Uenezi, Nape Nnauye (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari, leo
katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam,
kutoa tathmini ya matokeo ya awali uchaguzi wa Serikali za mitaa
uliofanyika juzi nchini kote.
No comments:
Post a Comment