Thursday, January 29, 2015

Mwakyembe afunguka


Dk Harisson Mwakyembe
Siku chache baada kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, waziri ambaye ameteuliwa kushika nafasi hiyo, Dk Harisson Mwakyembe amewataka Watanzania kuondoa hofu ya kuhamishwa kwake kutoka Wizara ya Uchukuzi, huku akisisitiza kuwa hana nia ya kugombea urais.

Dk Mwakyembe aliwataka wananchi kuondoa hofu kwa sababu utendaji aliouonyesha akiwa Wizara ya Uchukuzi, atauhamishia wizara yake mpya.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili muda mfupi baada ya kuapishwa na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Daniel Kidega, Mwakyembe alisema utendaji aliouonyesha katika wizara aliyokuwamo awali zamani, ndiyo uliomshawishi Rais Jakaya Kikwete kumhamishia Wizara ya Afrika Mashariki ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa masuala ya jumuiya hiyo.

"Watanzania wanapaswa kuondoa kasumba ya kutaka anayefanya vizuri katika nafasi yake kuendelea kubaki hapo hapo. Hapana! Anayefanya vizuri sehemu moja ni vyema akahamishiwa sehemu nyingine ili akafanye vizuri huko pia," alisema Mwakyembe na kuongeza:
"Ni utashi wa Mheshimiwa Rais kuamua kuwapanga wasaidizi wake kwa namna anayoona inafaa. Naamini utendaji wangu Wizara ya Uchukuzi ndiyo umesababisha nihamishiwe Afrika Mashariki ili niuendeleze huku pia."

Kauli ya Waziri Mwakyembe inakuja siku chache baada ya kutolewa kwa maoni ya wananchi yaliyoonyesha kutoridhishwa na uamuzi wa Rais kumbadilisha kutoka Wizara ya Uchukuzi kwenda Afrika Mashariki akibadilishana na Sitta aliyekwenda Wizara ya Uchukuzi.
Sina nia kugombea urais 2015

Akizungumzia malengo yake kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka huu, Mwakyembe alisema: "Akili na malengo yangu yote kwa sasa ni kutekeleza majukumu yangu kama Waziri wa Afrika Mashariki. Sina nia ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao. Hilo nawachia wenye nia hiyo," alisema.
Tayari wanachama kadhaa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wametangaza au kutajwa kwenye mbio hizo za urais.
Faida ya ushirikiano wa EAC

Akizungumzia faida za EAC, Waziri Mwakyembe alisema muda umefika sasa umma wa Afrika Mashariki uanze kupata faida ya moja kwa moja ya ushirikiano kati ya nchi wanachama za Tanzania, Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda akitaja nafuu ya gharama za usafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya kuangaliwa.
"Miaka 15 sasa imepita tangu kufufuliwa kwa jumuiya hii, lakini bado ni ghali kusafiri kwa ndege kati ya Dar es Salaam na Nairobi, Kampala, Bujumbura na Kigali kulinganisha na Johannesburg, Afrika Kusini, India au Dubai," alisema. Mwakyembe.
Chanzo:Mwananchi

No comments: