Mwenyekiti
wa Chama Tawala cha CCM,Rais Jakaya Mrisho Kikwete akilakiwa na maelfu
ya wananchi wakati akiingia katika uwanja wa MajiMaji mjini Songea leo
kuongoza kilele cha sherehe za kuadhimisha miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM.
Mwenyekiti
wa Chama Tawala cha CCM,Rais Jakaya Mrisho Kikwete akilakiwa viongozi
mbali mbali wa CCM wakati akiingia katika uwanja wa MajiMaji mjini
Songea leo kuongoza kilele cha sherehe za kuadhimisha miaka 38 ya
kuzaliwa kwa CCM.
Ndugu Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM;
Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu na mjumbe wa Kamati Kuu;
Mheshimiwa Anne Makinda, Spika wa Bunge na Mjumbe wa Kamati Kuu;
Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM;
Ndugu Mike Mukula, Makamu Mwenyekiti wa NRM ya Uganda na ujumbe wake;
Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati Kuu;
Mheshimiwa Oddo Mwisho, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma;
Waheshimiwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa;
Wajumbe wa Sekretarieti ya CCM;
Ndugu Verena Shumbusho, Katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma;
Wenyeviti wa Jumuiya za CCM;
Viongozi, wananchama na wapenzi wa CCM;
CCM Oyee!
Naomba
nianze kwa kuwashukuru na kuwapongeza wenyeji wetu kwa mapokezi mazuri,
hususan napenda kuwatambua wananchi, viongozi na wana-CCM wa Mkoa wa
Ruvuma wakiongozwa na Mwenyekiti wao ndugu Oddo Mwisho, Katibu wa Mkoa
Mama Verena Shumbusho, Mkuu wa Mkoa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa Ndugu
Said Mwambungu. Nawapongeza kwa maandalizi mazuri ya sherehe hizi.
Hakika zimefana sana. Hii ni mara ya pili sherehe hizi kuadhimishwa
mkoani hapa. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1991 wakati wa kuazimisha
miaka 14 ya CCM.
Tunatambua
kuwa mmefanya kazi kubwa ya maandalizi mpaka mmeweza kufanikisha
shughuli ya leo kwa kiwango cha juu. Waswahili wanasema "Usione vinaelea
Vimeundwa". Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi maalum kwa Katibu
Mkuu Abdulrahman Kinana kwa uongozi wake makini uliowezesha mambo kuwa
mazuri kiasi hiki. Hongera sana kwa hili na kwa kazi nyingi nzuri
unazofanya kwa maslahi ya Chama chetu na nchi yetu.
Leo ni
siku ya furaha kwangu na kwa viongozi na wanachama wenzangu wa CCM kote
nchini ya kusherehekea na kuadhimisha miaka 38 ya kuzaliwa kwa Chama cha
Mapinduzi. Tunastahili kuisherehekea siku hii kwa nderemo na vifijo kwa
sababu ya mafanikio makubwa ambayo Chama chetu kimeendelea kupata ndani
ya Chama na katika kuliongoza taifa letu. Katika miaka 38 ya uhai wake
Chama chetu kimezidi kuimarika na kimeendelea kuliongoza vyema taifa
letu: kuna amani, utulivu na maendeleo yanayoonekana.
Tumeeendelea
kuaminiwa na kutumainiwa na Watanzania. Kama ilivyothibitika na ushindi
wa kishindo katika chaguzi zote tangu mfumo wa vyama vingi uanze mwaka
1995 mpaka sasa. Hata mwaka huu itakuwa hivyo hivyo. Dalili ya mvua ni
mawingu: ushindi mnono tulioupata kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
ni dalili tosha kwamba Oktoba, 2015 watani zetu hawana chao.
Ninaposema
hivyo nawaomba wana CCM wenzangu tusibweteke tukadhani kwamba ndiyo
tumekwishafika. Bado safari ndiyo kwanza tumeianza na inaweza kuwa na
changamoto zake. Lazima tufanye kazi tena kazi kubwa sana ndipo
tutakapojihakikishia ushindi. Nguvu ya ushindi inaanzia kwenye Chama.
Huu ni mwaka ambao kazi ya Chama ndani ya Chama na kazi ya Chama ndani
ya umma inatakiwa ifanyike kwa nguvu zaidi na kwa ari kubwa zaidi.
Lazima tuhakikishe tunao umoja wa dhati na kwamba wanachama wetu
wanakuwa na mwamko wa hali ya juu wa kukipigania Chama katika kutafuta
na kupata ushindi kwa Udiwani, Ubunge, Uwakilishi, Urais wa Zanzibar na
Urais wa Muungano.
Huu ni
mwaka ambao wanachama na viongozi wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanakutana
mara kwa mara kwa mujibu wa Katiba na hata zaidi kuzungumzia mikakati
ya kupata ushindi na kuitekeleza. Huu ni mwaka ambao lazima tuhakikishe
kuwa tunazo rasilimali na nyenzo za kutuwezesha kufanya kazi ya Chama
ndani ya umma na kuwapatia ushindi wagombea wa Chama chetu.
Huu ni
mwaka ambao kazi ya Jumuiya za Chama ya kukiwezesha Chama kuungwa mkono
na jamii pana ya Watanzania walio vijana, wanawake na wazazi inafanyika
kwa umahiri na ufanisi wa hali ya juu.
Bila ya
shaka, ndugu zangu mtayakumbuka maneno niliyoyasema kwa kuyarudia kuwa
"Mwisho wa uchaguzi mmoja ndiyo mwanzo wa uchaguzi mwingine". Najua
baadhi yenu mmezingatia na kuchukua hatua za kufanya maandalizi mapema
ya uchaguzi wa mwaka huu mara baada ya kumaliza uchaguzi wa mwaka 2010.
Hao nawapongeza. Lakini wapo viongozi na wanachama ambao hawajafanya
chochote. Hawa, wananisikitisha kwa athari mbaya na hatari ya kupoteza
ushindi wanayokiletea Chama chetu.
Naomba
kila mmoja wetu ajipime yupo fungu gani. Kama upo kwenye kundi la kwanza
lililokwishaanza maandalizi natoa pongezi nyingi. Nawaomba muendelee
kukamilisha ipasavyo. Kwa wale ambao wapo kundi la wale ambao maandalizi
yao ni ya kiwango kidogo au hawajaanza kabisa lazima waanze na wakati
ni huu. Usikawie, unatakiwa kufanya kazi kwa ari zaidi, nguvu zaidi na
kasi zaidi kama ilivyo kauli mbiu ya CCM. Yapo mambo kadhaa ya kufanya
ambayo tulikwishaambiana tufanye. Miongoni mwao ni lile agizo la kutaka
kila ngazi ya Chama na hasa Wilaya na Mikoa kuwa na Mfuko wa Uchaguzi.
Wakati wake ndio huu sasa wa mfuko huo kufanya kazi iliyokusudiwa.
Naomba tujiulize wangapi wanayo mifuko hiyo na wangapi hawana. Kwa wale
walionayo wahakikishe ina rasilimali za kutosha. Kama hazitoshi waweke
mikakati ya kuitunisha mifuko hiyo. Kwa wale ambao hawajaanzisha wachune
bongo kuhusu namna ya kupata fedha za kuendeshea shughuli za uchaguzi.
Sina budi kuwatahadharisha kuwa msichukue fedha ambazo zitazua matatizo.
Ndugu viongozi na ndugu wanachama;
Huu ni
mwaka wa kutambua ahadi zipi tulizotoa zimetimizwa na zipi bado. Kwa
zile ambazo hazijakamilika wajibu wetu ni kuweka mikakati ya
kuzikamilisha. Kwa zile ambazo hazitakamilika tutafute maelezo sahihi ya
kutoa kwa wadau wa huduma hiyo. Naamini hazitakuwa nyingi za kuchosha.
Mwaka huu siyo mzuri kwenda na madeni lukuki ya ahadi. Yanaweza
kutupunguzia ushindi wetu.
Huu ni
mwaka wa kuongeza ukubwa wa jeshi letu la ushindi kwa kuongeza
wananchama wapya. Natambua tatizo la upungufu wa kadi lakini najua
mipango thabiti iliyopo ya kuleta kadi nyingi za kutosha wale waliopo
nje. Tujiepushe na kuingiza mamluki hivyo taratibu za kuingiza wanachama
zizingatiwe ipasavyo.
Ndugu Viongozi;
Ndugu Wananchi;
Jambo
lingine kubwa na muhimu sana kufanya mwaka huu ni kuwatembelea wanachama
na wananchi na kuzungumza nao. Hatujaifanya vizuri sana kazi hii lakini
hatujachelewa. Sina budi kutoa pongezi maalum kwa Katibu Mkuu wa CCM
kwa ufanisi mkubwa aliopata kwa jambo hili. Sote hatuna budi kuiga mfano
wake mzuri. Tuache kukaa maofisini tutoke kuzungumza na watu
kuwashawishi waunge mkono na kuipigia kura CCM katika uchaguzi ujao.
Kila Ofisi ya Mkoa na kila Ofisi ya Wilaya inalo gari la kuwawezesha
kufanya kazi hiyo. Tafadhali fanyeni hivyo, kwani bila ya kufanya hivyo
hakuna uhakika wa kupata ushindi. Kilichobakia kwa upande wetu ni
kutafuta vipando kwa Ofisi za Kata na Matawi. Tusaidiane pale
inapowezekana.
Uandikishaji wa Wapiga Kura
Ndugu wana CCM na ndugu Wananchi;
Jambo
lingine muhimu katika kutafuta ushindi ni kupatikana kwa wapiga kura.
Chama chetu kama vilivyo vyama vingine, hatuna budi kuwahimiza wanachama
wetu, wapenzi wetu na wananchi wengine wajitokeze kwa wingi
kujiandikisha kupiga kura. Mwaka huu wenye kadi mpya za mpiga kura ndiyo
watakaoruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi mkuu na katika kura ya
maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa.
Asiyejiandikisha
hatapata fursa ya kushiriki kura ya maoni na uchaguzi mkuu. Kwa sababu
hiyo nawaomba viongozi na wanachama wa CCM wawe ndiyo wa kwanza
kujitokeza kujiandisha. Pia wawe mstari wa mbele kuwahimiza wananchi
wengine kujiandikisha. Nawaomba jambo hili mlipe uzito mkubwa kwani
safari ya kutafuta na kupata ushindi inaanzie kwenye kupata wapiga kura
hususani wapiga kura wanaounga mkono Chama chetu na wagombea wetu.
Kura ya Maoni
Ndugu wananchi;
Kama
mjuavyo, jambo kubwa lililo mbele yetu ni kura ya maoni kuhusu Katiba
Inayopendezwa itakayofanyika tarehe 30 Aprili, 2015. Maandalizi yote
husika yanaendelea kufanyika ili kuwezesha kura hiyo kutekelezwa kama
ilivyopangwa. Kama nilivyokwishaeleza hivi punde uandikishaji wa wapiga
kura ni miongoni ma maandalizi hayo. Mengine ni uchapishaji na
usambazaji wa Katiba Inayopendekezwa.
Yapo
mambo kadhaa ambayo nawasihi viongozi na wanachama wenzangu mfuatilie
kwa karibu ili yasiwapite. Yale tunayoyajua tuwaambie. Miongoni mwa
mambo muhimu sana ambayo Chama hakina budi kujipanga vizuri ni kuhusu
kutoa elimu kwa umma kuhusu Katiba Inayopendekezwa na kampeni ya Kura ya
Maoni. Watani zetu watatoa elimu hasi kuhusu Katiba Inayopendekezwa,
sisi tutoe elimu chanya. Wenzetu watataka Katiba Inayopendekezwa
isipite. Sisi tupige kampeni ikubalike. Nilisema siku ileDodoma wakati
wa kukabidhiwa Katiba Inayopendekezwa na narudia tena leo kwamba Katiba
Inayopendekezwa imebeba maslahi mapana ya taifa letu. Hatujawahi kuwa na
Katiba kama hii Inayopendekezwa. Misingi ya historia ya nchi yetu yaani
kule tulikotoka, tulipo sasa na tuendako imezingatiwa vizuri. Katiba
hiyo inatambua maslahi ya makundi yote nchini na kuyawekea utaratibu
mzuri wa kutekelezwa. Wakulima, wafugaji, wavuvi, wanawake, vijana,
wasanii, wafanyakazi, wazee na watoto wametambuliwa kwa kina na upana
zaidi kuliko Katiba ya sasa.
Katiba
Inayopendekezwa imeshughulikia kero za Muungano na kujenga mazingira
bora zaidi kwa Muungano wetu kuimarika. Yale mambo yaliyokuwa yanaikwaza
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuukwaza Muungano yamepatiwa
ufumbuzi mwafaka. Sasa Zanzibar itaendesha na kushughulikia mambo yake
kwa uhuru mkubwa zaidi.
Ndugu wananchi;
Kwa maoni
yangu sioni sababu ya kuikataa Katiba Inayopendekezwa. Hatuna budi
kutambua kuwa tukiikataa Katiba Inayopendekezwa, Katiba ya sasa
itaendelea kutumika mpaka hapo mchakato mwingine utakapomalizika miaka
mingi ijayo. Viongozi wa vyama vinne vya siasa wamesikika wakisema
watasusia kushiriki katika kura ya maoni na kuwataka wanachama wao
wasishiriki. Kauli hiyo imenisikitisha sana ingawaje haikunishangaza
hasa tukikumbuka waliyoyafanya wakati wa Bunge la Katiba. Mimi nawaomba
washiriki.
Nawasihi
wananchi wasiwasikilize. Wao wakitaka kususia waacheni wasusie lakini
nyie jitokezeni kupiga kura. Nawasihi msikubali kupoteza mema mengi
yaliyo katika Katiba Inayopendekezwa ati kwa sababu tu hakuna Serikali
Tatu walizokuwa wanazitaka. Kama kweli wananchi wa Tanzania
wanakereketwa na Serikali Tatu watathibitisha hiyo kwenye kura ya maoni.
Naomba
msibabaishwe wala kudanganywa na watu wanaotaka kuturudisha nyuma kutoka
katika hatua kubwa muhimu tutakazopiga kwa kuikubali Katiba
Inayopendekezwa. Tusikubali kubaki nyuma.
Uchaguzi Mkuu
Ndugu wananchi;
Kama
mjuavyo mwezi Oktoba, 2015 nchi yetu itafanya uchaguzi mkuu wa Madiwani,
Wabunge, Wawakilishi, Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Uchaguzi wa mwaka huu ni wa kihistoria kwa nchi yetu kwani tunachagua
Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mimi nataka
Rais huyo awe mwana CCM. Sisi sote katika CCM tunataka Rais atoke katika
Chama chetu kwa sababu kama alivyousia Baba Wa Taifa Mwalimu Julius
Nyerere "Rais wa nchi yetu anaweza kutoka Chama chochote lakini Rais
bora atatoka CCM".
Huu ni
usia mzito wenye maono ya mbali. Tusiupuuze wosia huu bali tuuenzi. Sisi
katika Chama cha Mapinduzi tuwe mstari wa mbele katika kuuenzi wosia
huu kwa kupata mgombea aliye bora wa kupeperusha bendera ya CCM katika
uchaguzi ujao. Mgombea ambaye wananchi wakisikia jina lake likitajwa
watasema naam, hapo sawa, hapo barabara. Lakini tukiteua mgombea ambaye
watu wataguna na kusema hata huyu? Tutakuwa tumemuangusha Muasisi wa
Chama chetu na taifa letu katika wosia wake. Bila shaka laana yake
tutaipata. Na hilo likitokea itakuwa hasara kubwa kwa taifa letu na
msiba kwa CCM. Nchi itayumba.
Lazima
tuhakikishe kuwa hatutafika huko. Watu wazuri wapo wa kutosha katika CCM
na naamini tunawajua. Kama hawajajitokeza tuwashawishi wafanye hivyo.
Ndugu zangu, tusifanye ajizi katika jambo hili kubwa na la msingi kwa
Chama chetu. Kushinda chaguzi za dola katika sehemu zetu mbili za
Muungano ndiyo madhumuni makuu ya kuundwa na kuwepo kwa CCM.
Napenda
kuwahakikishia wanachama wa CCM na wananchi kuwa, Chama cha Mapinduzi ni
Chama kilichokomaa, kilicho makini na imara. Tunao utaratibu
unaoeleweka na kutabirika wa kuwapata wagombea. Inazo kanuni na vigezo
vya wazi vya kuwapata viongozi walio bora, na tunavyo vikao rasmi vya
kuchuja na kuteua wagombea kwa kuzingatia kanuni, taratibu na maadili ya
Chama chetu. Hivyo basi, hapataharibika jambo.
Naomba
niwahakikishie kwamba CCM itawapatia Watanzania wagombea bora ambao
hawatawapa wananchi mashaka wala kigugumizi cha kuwachagua. Tutafanya
hivyo kwa nafasi ya Rais wa Muungano, Rais wa Zanzibar, Wabunge,
Wawakilishi na Madiwani. Nawaomba wagombea wazingatie na kuheshimu
masharti ya Katiba ya Chama, Kanuni na Madili ya uteuzi kwa wanaotaka
kuteuliwa kugombea nafasi katika chaguzi za dola. Asiyezingatia hayo
asije akakilaumu Chama bali ajilaumu mwenyewe kwa makosa aliyoyafanya.
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa CCM
Ndugu wananchi;
Miezi
minne iliyopita nilifanya ziara ya mkoa huu wa Ruvuma kukagua shughuli
za maendeleo. Nimefurahishwa sana na jitihada za kujiletea maendeleo
zinazofanywa na wananchi wa mkoa huu na mafanikio mnayoendelea kuyapata.
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na mipango mbalimbali ya
serikali unakwenda vizuri, kiasi cha kuwastajabisha hata wale waliokuwa
na mashaka na wasio tutakia mema.
Yako
mambo mengi tuliyoahidi kufanya ambayo tumeyakamilisha na mengine
utekelezaji wake unaendelea vizuri. Kilio cha miaka mingi cha wananchi
wa mkoa huu kuhusu barabara kimefanyiwa kazi vya kutosha. Ujenzi wa
barabara ya Namtumbo – Songea na Peramiho - Mbinga kwa kiwango cha lami
umekamilika. Tunaendelea na ujenzi wa barabara ya Namtumbo – Tunduru na
Tunduru – Mangaka ili kuunganisha mkoa wa Mtwara na Ruvuma kwa barabara
za lami. Aidha, mipango ya kujenga barabara ya Mbinga – Mbambabay kwa
mkopo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika imefikia mahali pazuri. Kwa upande
wa usafiri katika Ziwa Nyasa hivi sasa mchakato wa ujenzi wa chelezo
cha kujengea meli ya ziwa hilo kule kwenye bandari ya Itungi, Kyela
unaendelea vizuri. Ujenzi wa chelezo ukishakamilika ujenzi wa meli
utaanza.
Kwa
upande wa umeme tunaendelea na ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa Kv
220 kutoka Makambako kuja Songea na hadi Mbinga na Namtumbo. Ujenzi wa
njia hii ya umeme utakapokamilika utawahakikishia wakazi wa mji wa
Songea na mkoa wa Ruvuma umeme wa uhakika. Tumechelewa kidogo kwa sababu
ya kubadilisha ukubwa wa njia kutoka msongo wa Kv 132 tuliyotaka
kujenga awali hadi Kv 220. Aidha, usambazaji wa umeme vijijini
unaendelea kwa kasi katika maeneo yote nchini. Tunataka ifikapo June,
2015 zaidi ya vijiji 5,336 viwe vimepatiwa umeme. Kati ya vijiji hivyo
zaidi ya vijiji 300 ni vya mkoa wa Ruvuma. Haya ni mafanikio makubwa na
ya kutia moyo.
Kuhusu
sekta ya Afya nako pia tumepata mafanikio makubwa katika utoaji wa
huduma ya afya kwa Watanzania. Kwa hapa Songea nimekwishatoa maelekezo
kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuanza mchakato wa ujenzi wa
hospitali mpya ya Mkoa wa Ruvuma na hii iliyopo sasa iwe ni hospitali ya
Manispaa ya Mji wa Songea. Halmashauri ya Manispaa ya Songea iharakishe
kutenga eneo la kutosha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo ya mkoa
ambayo itakuwa ni ya rufaa kwa yale ambayo hospitali za Wilaya
zitashindwa kumudu.
Haya ni
maeneo machache tu ambayo yanaonyesha hatua kubwa tuliyopiga katika
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na maendeleo ya mkoa huu. Ukweli ni
kwamba Ruvuma ya miaka 10 iliyopita siyo Ruvuma ya leo. Ninyi nyote ni
mashahidi wa mambo haya. Mwenye macho haambiwi tazama.
Ndugu wananchi;
Jambo la
mwisho ambalo napenda kulizungumzia ambalo nilishalizungumzia kwenye
hotuba yangu ya mwaka mpya inahusu ununuzi wa mazao ya wakulima.
Nilieleza siku ile kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)
ilikuwa bado haijalipa shilingi bilioni 89 kwa wakulima kwa mazao yao
iliyonunua. Nilielezea kutokufurahishwa kwangu na hali hiyo na kuagiza
Wakala kulipa deni hilo.
Nimeambiwa
kuwa tayari shilingi bilioni 15 zimeshatolewa na hapa Ruvuma mmepata
shilingi bilioni 8. Hivi karibuni shilingi bilioni 36 zitatolewa na
kubaki shilingi bilioni 38 ambazo zitalipwa mwezi Machi.
Jambo
lingine ambalo tunaendelea nalo kulishughuikia katika Serikali ni kupata
masoko mengine kwa mazao ya wakulima. Kama nilivyosema NFRA haiwezi
kununua mazao yote ya wakulima nchini. Uwezo wake ni kuhifadhi tani
240,000 wakati uzalishaji wa mahindi hapa Ruvuma ni tani 993,350. Hata
kama NFRA ingeamua kununua mahindi yote kutoka mkoa wa Ruvuma peke yake
isingeweza kuyamaliza.
Nimewaagiza
viongozi wa mkoa wa Ruvuma na mikoa yote nchini washirikiane na Wizara
ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Wizara ya Viwanda na Biashara kutafuta
masoko mengi kwa ajili ya mahindi, mpunga na mtama wa wakulima ndani na
nje ya nchi.
Tunakokwenda
Ndugu wana CCM;
Mafanikio
ya miaka 38 ya Chama chetu yasitufanye tubweteke. Bado tunayo kazi
kubwa mbele yetu. Ili tuendelee kuongoza dola hatuna budi tuendelee kuwa
tumaini na kimbilio la wananchi wetu. Inatupasa kuwa waaminifu kwa
ahadi zetu na watiifu kwa matakwa yao. Kubwa sana, tunatakiwa tuwe
tayari wakati wote kubadilika na kwenda na wakati. Tunaweza kufanya
hivyo ikiwa tutaendelea kukuza demokrasia ndani ya Chama chetu na
kuruhusu na kuvumilia tofauti za mitazamo. Hiyo ndiyo siri ya uhai wa
CCM ambayo hatuna budi kuendeleza.
Tunapoanza
safari ya kuelekea mwaka wa 39, hatuna budi sasa kuelekeza nguvu zetu
kwenye kuondoa utegemezi wa kifedha kutoka kwenye ruzuku na michango ya
wafanyabiashara. Kutegemea misaada na michango si mambo endelevu na huo
hauwezi kuwa ni mkakati wa kutumainiwa wa kuimarisha Chama chetu. Wakati
mwingine michango hii imetugharimu ndani ya Chama chetu. Lazima tuwe
wabunifu katika kutafuta vyanzo vya mapato ikiwa ni pamoja na rasilimali
zetu nyingi tulizonazo ili kuwezesha Chama kujitegemea. Tayari yako
mawazo yaliyoibuliwa kutokana na kazi nzuri ya Kamati iliyoongozwa na
Mjumbe wa Kamati Kuu na Mweka Hazina wetu Mheshimiwa Zakhia Meghji
tumeagiza yatekelezwe. Naomba mtimize ipasavyo wajibu wenu.
Hitimisho
Ndugu wana CCM;
Leo ni
siku ya furaha kwetu sote. Wakati tukisherehekea mafanikio yetu
tuwakumbuke pia waasisi wetu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyekuwa
Mwenyeti wa TANU na Ndugu Sheikh Aboud Jumbe aliyekuwa Mwenyekiti wa
ASP kwa busara, hekima na uamuzi wao uliotukuka uliowezesha kuzaliwa kwa
CCM. Tunawakumbuka pia wale wote waliotangulia mbele ya haki ambao
walijitoa maisha yao kujenga CCM. Hatuna budi kuwaenzi kwa kutoa mchango
mkubwa zaidi mwaka ujao na miaka mingi ijayo. Tuhakikishe kuwa
tunaimarisha Chama chetu na kutenda mema kwa ajili ya nchi yetu na watu
wake. Hili linawezekana ikiwa kila mtu atatimiza wajibu wake. Kidumu
Chama cha Mapinduzi!
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment