VIONGOZI
wa dini za Kiislamu na Kikristo nchini wamekubaliana kutoandaa mihadhara
inayokashifu dini moja na nyingine, miongoni mwa madhehebu ya dini moja
au kashfa baina ya waumini na waumini.
Lengo la
makubaliano hayo ni kudhibiti madhara ya mihadhara hiyo ambayo
imeonekana inachangia uchochezi wa ugaidi na uvunjifu wa amani.
Katibu
Mkuu wa Taasisi ya Mashehe na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Shehe
Hamis Mataka aliyasema hayo jana Dar es Salaam, wakati akifungua
kongamano la siku mbili lililoandaliwa na Iman Burkhary Islamic
Foundation, linalojadili madhara ya misimamo mikali ya imani za dini.
Shehe
Mataka alisema kwamba viongozi wa dini zote wasimame imara kukemea watu
wanaojitokeza kuchochea uvunjifu wa amani kupitia dini.
Alisema
kwamba wapo watu wanaotumia dini kujipatia maslahi yao binafsi, badala
ya kuwafundisha watu kufuata mafundisho sahihi ya Mungu kwa kuhimizana
upendo na amani.
‘’Kongamano
hilo limekuja wakati sahihi kuangazia yaliyo ndani ya nchi yetu. Sisi
Waislamu hatuna tatizo na Wakristo nao vivyo hivyo hawana tatizo na sisi
kwa sababu sote tunatambua uwepo wa dini zote,’’alisema Shehe Mataka.
Alisema
kuwa mafunzo yasiyo sahihi na upotoshwaji wa dini unaofanywa na baadhi
ya watu unatakiwa kukemewa kwa nguvu zote ili uovu utokanao na
upotoshwaji huo usije kuiangamiza nchi.
Aliongeza
kuwa endapo hakutakuwa na mihadhara inayochochea hasira na uvunjifu wa
amani nchini, viongozi hao wa dini wataweza kuwakemea viongozi waliopo
serikalini watakaokiuka maadili.
“Ikigundulika
mtu anasimama na kupotosha mafundisho ya dini ni lazima tusimame kidete
kumkataa mtu huyo kwani hafai kwa kuwa anachochea mauaji,” alisisitiza.
Kwa
upande wake, Askofu wa Kanisa la Galilaya Temple lililopo Msasani, Dk
Philbert Mbepera aliwaasa viongozi wenzake kutobeza dini hata kama mtu
ataonekana kuuabudu mti. Dk Mbepera alisema amani ya nchi hii haiwezi
kujengwa na watu wengine bali kwa kuhamasishana upendo na kuvumiliana.
Alisema
waumini wasilazimishane kuamini dini fulani bali kuelekezana na kuonyana
wanapokosea. Pia alisema wameanza kufanya maombi ya siku 40 kuombea
amani ya nchi kwani bila ya kufanya hivyo madhara makubwa yanaweza
kutokea.
Hata
hivyo, Shehe wa Masjid ya Qhadir Kigogo Post, Hemed Jalala alisema
kwamba viongozi wa dini watasaidia katika kuwaelimisha vijana juu ya
madhara ya ugaidi na ukatili.
Alisema
endapo vijana hao wataendekeza ugaidi ambao unainyemelea nchi,
hawatakuwa salama na watavuruga amani ya nchi. Aliwaasa vijana
kuvumiliana katika kila hali na kwamba wanasiasa watakaokwenda kombo
watawekwa chini na kukemewa.
No comments:
Post a Comment