Waziri wa
Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli amesema serikali itajenga barabara ya
Igawa hadi Ubaruku KM 18 kwa kiwango cha lami ili kuinua fursa za uchumi
za wilaya ya Mbarali na kuwezesha magari makubwa kupita kwa urahisi
kufuata mazao katika eneo hilo.
Waziri
Dkt. Magufuli amesema hayo katika ziara yake inayoendelea mkoani Mbeya
ambapo leo ameweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara ya igawa-ubaruku
yenye urefu wa KM 18 na kusisitiza barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi wa
mkoa wa Mbeya na taifa kwa ujumla.
"Nitahakikisha
barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami na kukamilika mapema ili
kuunga mkono juhudi za wananchi wa Mbarali wanaotekeleza sera ya kilimo
kwanza kwa kuzalisha mpunga na mahindi kwa wingi", amesisitiza waziri
Magufuli.
Amewataka
wananchi waliojenga katika hifadhi ya barabara kupisha eneo la barabara
ili kuwezesha kazi ya ujenzi huo kufanyika kwa haraka na kumalizika kwa
wakati.
Amemwagiza
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini TANROADS Eng. Patrick
Mfugale kufanya usanifu ili kuwezesha madaraja kumudu kupitisha magari
yenye uzito wa tani 40 yatakayochukua mazao katika maeneo ya Rujewa na
Ubaruku.
Eng.
Mfugale amesema barabara ya Igawa-Ubaruku kwa sasa ni barabara ya mkoa
na ujenzi wake utazingatia vigezo vya barabara za mikoa ili kukidhi
mahitaji ya uzito wa magari yatakayopita katika barabara hiyo.
Kuhusu
barabara ya Igawa –Madibira yenye urefu wa KM 153 ambayo upembuzi
yakinifu na usanifu wake umekamilika waziri Magufuli amesema Serikali
inatafuta fedha ili kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami na hivyo
kuifungua kiuchumi wilaya ya Mbarali.
Amesisitiza
umuhimu wa umoja,mshikamano na uaminifu kwa wananchi wa Mbarali na
kuwataka vijana watakaopata kazi wakati wa ujenzi wa barabara hiyo kuwa
waaminifu.
Naye mkuu
wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro amemshukuru Waziri wa Ujenzi kwa kuamua
kujenga kwa lami barabara za Mpemba hadi Isongole wilayani Ileje ,Igawa
hadi Ubaruku wilayani Mbarali na Kikyusa hadi Matema wilayani Kyela na
kusisitiza barabara hizo zitakapokamilika zitaimarisha usafiri na kuibua
fursa za ajira na uchumi kwa wakazi wengi wa mkoa wa Mbeya.
No comments:
Post a Comment