Baraza la
Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na
burudani nchini linawakumbusha wamiliki na waendeshaji wa kumbi za
burudani kufuata sheria, kanuni na taratibu walizopewa kwenye vibali
vyao vya uendeshaji wa kumbi.
Wanaelekezwa
kuhakikisha wanakuwa na vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao,
kuzingatia muda wa utumizi wa kumbi, kuepuka kelele zinazosumbua kwenye
maeneo maalum hasa makazi ya watu na kuhakikisha ulinzi na usalama wa
maisha ya watu.
Aidha,
BASATA linawakumbusha wamiliki wote wa kumbi za burudani kwamba ni
marufuku kukusanya watoto katika kumbi zao kupitia kile kinachoitwa
'Disko Toto' ili kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza.
Uzoefu
unaonesha kwamba, nyakati za sikukuu kama hizi wamiliki wa kumbi
wamekuwa wakijisahau na kumezwa na faida katika biashara zao kiasi cha
kuandaa madisko ya watoto hali mbayo imekuwa ikisababisha maafa makubwa
ambayo yangedhibitika kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.
BASATA
kama mtoaji wa vibali vya kumbi za sherehe na burudani linasisistiza
kwamba halitafumbia macho ukumbi wowote utakaokiuka maelekezo haya
sambamba na kuruhusu maonesho machafu yenye kudhalilisha utu wa binadamu
hasa yale yanayoonesha maungo ya ndani. Hatua kali na za kisheria
zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka maagizo haya.
BASATA linawatakia wasanii na wadau wote wa Sanaa sherehe njema ya Pasaka yenye furaha tele.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI
KATIBU MTENDAJI
No comments:
Post a Comment