Sunday, April 5, 2015

SALAM: Naye Yesu Akasema; " Simoni, Acha Kuvua Samaki.."


2_7ea4d.jpg

Ndugu Zangu,
Bwana Yesu alipotembelea mto Galilaya, aliwakuta wavuvi wakivua samaki, Simoni alikuwa ni miongoni mwa wavuvi hao. Yesu akasema; " Simoni, acha kuvua samaki,nifuate ukawe mvuvi wa watu.
Naam, watu wengi wanaangamia kwa kukosa uelewa. Kwa kutojitambua. Wanahitaji ukombozi wa kifikra. Na siku zote, haki uinua taifa, vivyo hivyo, dhulma huangamiza taifa. Na mahala pasipo na haki, basi, hapo hapatukuwa na amani.
Oneni, maovu yametamalaki katika dunia tunamoishi. Siku zote, kujipendelea ndilo shina la maovu.
Siku zote, hamu inakuwa ni jambo jema, endapo binadamu ataweza kuitawala hamu/tamaa yake.Wanadamu tusipoitawala hamu yetu, tukaanza kujipendelea, kuwasahau wengine, basi, hilo huwa ndio chimbuko la maovu.
Hupelekea kutoelewana baina ya wanandugu, na hata kwa marafiki walioshibana. Hupelekea vurugu na machafuko katika jamii. Tunazungumzia uwepo wa upendo, haki na usawa.
Dini za kweli hapa duniani zinazungumzia umuhimu wa upendo, haki na usawa katika jamii. Iwe ni Uislamu na Ukristo vivyo hivyo.
" Naapa kwa zama . Hakika binadamu wote wamo katika hasara isipokuwa wale walioamini na wakafanya matendo mema. Wakahusiana na haki na wakahusiana na subira" (Koran tukufu, Surat ASWR)
Biblia nayo inasema; kuwa Kaini alikuwa mtu wa kujipendelea mno, akamwua nduguye. Mfalme Saulo alijipendelea mno, akamdhulumu Daudi. Yuda alijipendelea mno, akakubali kumsaliti Yesu kwa Vipande Thelathini vya Fedha. Hatimaye, akamsaliti Yesu.
Na ufufuko wa Bwana Yesu utukumbushe jukumu letu la kupambana na maovu katika jamii. Utukumbushe jukumu la kusaidia kazi ya kuwakomboa kifikra wanadamu wenzetu.
Kama vile Bwana Yesu alivyomkumbusha Simoni kwa kumwambia; " Simoni, acha kuvua samaki. E nenda ukawe mvuvi wa watu.
Ni Neno la Leo.
Pasaka Njema.
Maggid,
Iringa.

No comments: