Masanja Mwinamila (44) mara baada ya kufikishwa katika kituo cha Polisi Wilaya ya Nzega Juni 15, 2015.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, ACP Juma Bwire akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo Juni 16, 2015.
MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Nzega leo hii imemhukumu Masanja Mwinamila
(44), mkazi wa Kitongoji cha Kona Nne, Kijiji cha Ugembe II, Kata ya
Mwakashanhala, Tarafa ya Puge wilayani Nzega katika Mkoa wa Tabora
kwenda jela miaka 10 kwa kosa la kuteka mtoto mwenye albinism, Margreth
Hamisi (6).
Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Saraphine Nsana, alitoa hukumu hiyo
baada ya mshtakiwa kusomewa shtaka na kukiri kutenda kosa hilo.
Ilielezwa
mahakamani hapo kwamba, mnamo Juni 15, 2015 majira ya saa 3:00 usiku
katika Kijiji cha Ugembe II, Kata ya Mwakashanhala wilayani Nzega,
mtuhumiwa alimteka binti huyo kwa lengo la kwenda ‘kumuuza’ ili ajipatie
fedha (kiasi kimehifadhiwa).
Hii ni
mara ya kwanza kwa kesi inayohusisha utekaji nyara, kujeruhi na mauaji
dhidi ya watu wenye albinism kuchukua muda mfupi zaidi, kwani ndiyo
kwanza kesi hiyo ya Jinai Namba 116/2015 imefikishwa mahakamani kwa mara
ya kwanza na kutolewa hukumu.
Mafanikio
ya kukamatwa kwa Masanja Mwinamila akiwa katika harakati za kutaka
kumuuza mtoto Margreth Hamisi, ambaye ni mpwa wake, yametokana na
umakini wa Jeshi la Polisi nchini ambapo maofisa wake wa Kikosi Kazi cha
Taifa waliweka mtego na kufanikiwa kumnasa mtuhumiwa kabla hajamdhuru
mateka wake.
Tukio
hilo limefanikisha kuubomoa mtandao hatari wa mauaji ya watu wenye
ulemavu wa ngozi (albino) kwani ni takriban wiki tatu tu tangu maofisa
usalama walipofanikiwa kuwanasa watu wengine sita wakiwa katika harakati
za kuuza mifupa inayodhaniwa kuwa ya binadamu (albino) mjini Kahama Mei
22, 2015 ambapo tayari wamekwishafikishwa mahakamani pamoja na wengine
watatu waliokamatwa baadaye.
Matukio
hayo mawili makubwa yaliyotokea katika kipindi hicho yamedhihirisha
namna serikali kupitia jeshi hilo na vyombo vingine vya usalama
inavyoshughulikia mitandao hiyo hatari usiku na mchana ili kuhakikisha
Watanzania wote wanaishi kwa amani na usalama.
No comments:
Post a Comment