Friday, September 18, 2015

MBEYA CITY ILIVYOTAKATA NYUMBANI, YAIBUGIZA BILA HURUMA JKT RUVU

Kikosi cha Mbeya City - 2015

Wachezaji wa Mbeya Citu wakishangilia moja ya magoli yao
  
BAADA ya kupoteza mchezo wa ufunguzi katika uwanja wake wa nyumbani kwa kukubali kipigo cha goli moja kwa nunge jumapili iliyopita dhidi ya Kagera Sugar,Timu ya Mbeya city  imesawazisha makosa kwa kuibugiza bila huruma timu ya Ruvu JKT ya Pwani.
 
Ikicheza mbele ya mashabiki wachache katika raundi ya pili ya ligi kuu Vodacom, Mbeya city ilifuta makosa ya raundi ya kwanza kwa kuifunga JKT Ruvu magoli matatu kwa bila.
 
Mshambuliaji wa Mbeya City Joseph Mahundi aliwainua mashabiki wake dakika ya 23 baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira uliopigwa kutoka wingi ya kulia na Shamte Ally na kumshinda mlinda mlango wa JKT Ruvu Tonny Kavishe, goli lililodumu hadi mapumziko.
 
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu lakini washambuliaii wa JKT Ruvu hawakuwa makini na mipira yao kuishia kwa mlinda mlango mkongwe nchini Juma Kaseja aliyetua Mbeya City msimu huu.
 
Themi Felix aliipatia timu ya Mbeya city goli la pili kwa njia ya mkwaju wa penati mnamo dakika ya 56 baada ya mlinda mlango wa JKT Ruvu kumdaka mguu mshambuliaji wa Mbeya City Geophrey Mlawa.
 
Jkt Ruvu walionekana kuzidiwa maarifa na timu ya Mbeya city baada ya dakika ya 70 mshambuliaji David Kabole kuhitimisha kalamu ya magoli kwa kufunga goli la tatu baada ya kupokea pasi kutoka kwa Joseph Mahundi aliyeambaa na mpira hadi kumfikia mfungaji.
 
Timu zote mbili zilifanya mabadiliko ambapo timu ya Mbeya city iliwatoa Abubakari Mwijuma, Them Felix na Geophrey Mlawa  na nafasi zao kuchukuliwa na Meshack Samwel, David Kabole na Hamad Kibopile.
 
Na upande wa JKT Ruvu waliwatoa Gaudence Mwaikimba, Issa Ngao na Amos Edward na nafasi zao kuchukuliwa na Samwel Kumuntu, Emmanuel Pius na Musa Ndiyunza.
 
Hadi kipenga cha mwisho kutoka kwa mwamuzi wa kati mwenye beji ya Fifa, Frolentina Zabron kutoka Dodoma, Mbeya city 3 na JKT Ruvu 0.

No comments: