BAADA ya
kufika kwa gesi asilia jijini Dar es Salaam ikitokea Mtwara, Shirika la
Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya
Petroli Tanzania (TPDC), itaingiza gesi hiyo katika mitambo yote ya
umeme nchini, hivyo kuanzia leo kutakuwa na ukosefu wa umeme katika
mikoa yote inayotumia Gridi ya Taifa.
Hatua
hiyo inatokana na kuzimwa mitambo yote ya umeme katika kituo kikubwa cha
kuzalisha umeme cha Ubungo, Dar es Salaam kwa nia ya kuingiza gesi
asilia katika mitambo huo. Imeelezwa kuwa tatizo hilo la umeme, litadumu
kwa wiki nzima ambao umeme utakatika kwa saa kadhaa usiku na mchana,
lakini hali itakuwa mbaya zaidi kwa siku ya leo.
Akizungumza
katika kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi One jana, Mkurugenzi
Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema mitambo yote ya umeme
itazimwa ili kuingiza gesi asilia kuanza kuzalisha umeme katika kituo
hicho kikubwa.
“Wiki hii
umeme utakatika sana kutokana na kuunganishwa gesi kutoka Mtwara kwa
ajili ya kuzalisha umeme kwa kuanzia kesho mitambo yote itazimwa,”
alisema Mramba. Alisema kwa saa za mchana na usiku ndani ya wiki hii
itakuwa mikoa yote inayotumia Gridi ya Taifa itakosa umeme.
Alisema
baada ya majaribio ya kupitisha gesi asilia kukamilika sasa wanaingiza
kwenye mitambo hiyo ili kuanza kuzalisha megawati 150 za umeme huku
mitambo ya megawati 200 iliyokuwa haifanyi kazi kutokana na gesi
kutotosha nayo itaanza kufanya kazi.
Alisema
baada ya kuunganisha bomba hilo na umeme kuanza kuzalishwa mwishoni mwa
wiki Watanzania watakuwa na uhakika wa umeme pamoja na bei ya umeme ya
uhakika kwa muda mrefu.
No comments:
Post a Comment